Wednesday, April 18, 2018

Serikali Kuajiri Walimu 6,000 June

 
 
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imesema hadi kufikia Juni 30 mwaka huu inatarajia kuajiri walimu 6,000 wa masomo ya Hisabati na Sayansi kwa ajili ya shule za sekondari nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali, ambaye alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuondoa changamoto katika shule za kata ikiwamo upunguzu wa walimu wa Hisabati na Sayansi.

Pia, Bobali alitaka kujua msimamo wa serikali kuhusu wananchi kuchangia kwenye chakula ambacho wameona ndio chachu ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika Mkoa wa Lindi. Alisema hadi Desemba mwaka 2017, Serikali ilikuwa imeajiri walimu 200 wa Hisabati na Sayansi kwa ajili ya shule za sekondari.

Kadhalika, alisema serikali haijazuia wananchi kuchangia maendeleo ya shule walichokataza ni kumzuia kumpa adha ya kukosa masomo mwanafunzi ambaye ameshindwa kuchangia michango hiyo.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua kama serikali imefanya tathmini juu ya ubora na changamoto zilizopo katika shule za sekondari za kata nchini.

Akijibu Kakunda alisema hadi Oktoba 2017, Shule za kata 3,103 zilikuwa na wanafunzi 197,663 ambao kama zisinge kuwepo wangeikosa elimu ya sekondari.

Kakunda alisema maamuzi ya kuanzishwa kwa shule ya sekondari kila kata ili kuhakikisha watoto wengi zaidi waliokuwa wanakosa nafasi za masomo ya sekondari licha ya kufaulu mitihani ya darasa la saba kwa sababu tu ya uchache wa shule wanapata nafasi hizo.

Alisema tathmini mbili za serikali zilizochambua kwa kina sekta ya Elimu kupitia Tume ya Prof. Mchome ya mwaka 2013, iliyochambua sababu za ufaulu hafifu wa wanafunzi kwenye mitihani ya mwaka 2012 na kamati ya kuhuisha na kuoanisha sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya mwaka 1996.

Pia alisema sera ya Taifa ya Elimu ya juu ya mwaka 1999 na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa elimu ya msingi ya mwaka 2007, iliyoongozwa na Mwalimu Abubakar Rajab mwaka 2013, ndizo zilizobaini na kuishauri serikali kuanzisha sera mpya moja ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.

“Sera mpya imetoa maelekezo mahususi kuhusu namna ya kuboresha elimu ya awali, msingi, sekondari, elimu ya ufundi na elimu ya juu na mitaala imesharekebishwa, ikama, vifaa, samani na miundombinu vyote vinaendelea kuboreshwa,” alisema.

Mvua zaendelea kuleta madhara nchini




 Mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbali mbali nchini zimeendelea kuleta madhara mkoani Rukwa, ambapo zimesababisha uharibifu wa mashamba ya vyakula na kuharibu mazao.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Rukwa, George Kyando ambapo amesema kuwa mvua hizo zimezoa mazao kwenye mashamba mkoani humo na mengine kuyafunika kwa udongo, hali ambayo imeleta hasara kwa wakulima.

Kamanda Kyando amesema kuwa barabara mbalimbali zimekatika na kukosa mawasiliano, huku baadhi ya madaraja yakizolewa na maji lakini hakuna taarifa ya vifo waliyoipata mpaka sasa.

“Huku Rukwa kuna barabara inayopita bonde kwa bonde kutoka mkoa wa Rukwa kwenda Katavi, kutokana na hizi mvua zinazonyesha madaraja yamechukuliwa na maji, barabara zimekatika, mashamba ya mipunga na mahindi yamefunikwa na udongo, kwa hiyo tumepata hayo majanga lakini tunashukuru Mungu hakuna mtu yeyote ambaye amedhurika na hiyo mvua, ni miundombinu na mashamba tu,”amesema Kyando

Hata hivyo, kutokana na mvua hizo Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania imewataka wananchi kuwa makini wanaposafiri na kutembea, kwani mvua kubwa zaidi inatarajiwa kunyesha siku za hivi karibuni.

Mke wa aliyekuwa Rais wa Marekani George H W Bush Afariki Dunia

 

Mke wa rais wa 41 wa Marekani, George H W Bush, mama Barbara Bush ambaye pia alikuwa mwanaharakati amefariki dunia.


Mama Bush ambaye pia ni mama wa rais wa zamani wa Marekani, George W Bush amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 92.

Taarifa ya kifo chake ilitolewa na ofisi ya rais, George H W Bush na ilieleza kuwa kifo chake kimetokana na matatizo ya kiafya.

Aidha, mara kadhaa mama Bush alilazwa hospitalini mara kwa mara ambapo siku ya Jumapili aliamua abakie nyumbani akiwa na familia yake.

Januari mwaka 2017, yeye na mumewe rais mstaafu Bush walilazwa kwa wakati mmoja. Yeye alikuwa akitibiwa kutokana na matatizo ya koo, huku mumewe akitibiwa kwa ugonjwa wa nimonia.

Mama Bush ni mmoja kati wanawake wawili tu nchini Marekani, kuwahi kuwa mke wa rais na mama wa rais. Abigail Adams alikuwa mke wa John Adams, na mama wa rais John Quincy Adams, rais wa sita wa Marekani.

Wachunguzi wa sumu Hatimaye Wameruhusiwa Kuingia Syria




Wachunguzi wa kimataifa leo Aprili 18 wameingia katika mji wa Syria uliokumbwa na kile kinachodaiwa kuwa ni shambulizi la sumu.

Hata hivyo, wachunguzi hao wanaingia nchini humo ikiwa ni  siku kadhaa za kucheleweshwa na onyo kutoka kwa mataifa ya magharibi kuwa ushahidi muhimu huenda umeshaondolewa.

Shirika la habari la Syria - Sana limesema wataalamu  hao kutoka Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Silaha za Sumu -OPCW wameingia mjini Douma.

Shambulizi hilo linalodaiwa kuwa la gesi mnamo Aprili  7 mjini Douma, karibu na Damascus, liliripotiwa kuua zaidi ya watu 40.

Mataifa ya magharibi yalimtuhumu Rais wa Syria Bashar al-Assad kwa tukio hilo.

 Watalaamu hao waliwasili Syria siku ya mashambulizi ya nchi za magharibi lakini wakazuiwa kuingia Douma.

SAMATTA ABADILISHWA BAADA YA SAA MOJA GENK IKITOA SARE YA 0-0 UGENINI

Image result for samattaMSHAMBULIAJI wa kimataifa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa Jumanne amecheza kwa dakika ya 65, klabu yake, KRC Genk ikilazimisha sare ya 0-0 na wenyeji, AA Gent katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Ghelamco-Arena mjini Gent.
Samatta alipambana kwa dakika zote 65 kabla ya kubadilishwa, nafasi yake ikichukuliwa na mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis ambaye naye hakuweza kwenda kubadili matokeo.
Hiyo inakuwa mechi ya 83 kwa Nahodha huyo wa Taifa Stars, Samatta tangu alipojiunga na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 

Na katika mechi hizo, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
Kikosi cha AA Gent kilikuwa; Kalinic, Gigot, Verstraete, Christiansen/Chakvetadze dk79, Janga/Kalu dk45, Yaremchuk, Dejaegere/Andrijasevic dk45, Asare, Bronn, Simon na Foket.
KRC Genk; Vukovic, Uronen/Nastic dk43, Colley, Aidoo, Maehle, Seck, Malinovskyi, Pozuelo, Trossard, Samatta/Karelis dk65 na Ndongala/Buffel dk84.

KILA LA HERI YANGA SC; MUNGU IBARIKI TIMU YETU IFUZU HATUA YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO

Image result for yanga 
YANGA SC inateremka Uwanja wa Hawassa mjini Hawassa, Ethiopia kuanzia Saa 10:00 jioni ya leo kwa saa za Tanzania kumenyana na Welaita Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa marudiano wa mchujo kuwania tiketi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga inaingia kwenye mchezo wa leo, ikiwa na mtaji wa ushindi wa mabao 2-0 iliyooupata kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Aprili 7, mwaka huu.
Lakini tu, kocha aliyeiongoza Yanga kupata ushindi huo, George Lwandamina amekwishaondoka amerejea klabu yake ya zamani, Zesco United na sasa timu ipo chini ya waliokuw wasaidizi wak Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazawa Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali, kocha wa makipa.
 Katika mchezo wa leo, Yanga itaongezewa na nguvu na wachezaji wake wanne waliokosekana kwenye mechi ya kwanza sababu ya adhabu za kadi za njano, mabeki Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na mshambuliaji Obrey Chirwa.
Wolaita Dicha nayo itaongezewa nguvu na wachezaji wao wawili, Teklu Tefesse Kumma na Eshetu Mena Medelecho baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kila mmoja katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Zamalek ya Misri.
Welayta Dicha imefika hatua hii baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 3-3, kila timu ikishinda 2-1 nyumbani kwake, wakati Yanga SC imetolewa Ligi ya Mabingwa baada ya kufungwa 2-1 na Township Rollers ya Botswana Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam Machi 6 katika mchezo wa kwanza wa 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kwenda kupata sare ya 0-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Gaborone nchini Botswana.
Katika Raundi ya Awali ambayo Yanga SC iliitoa Saint Louis Suns United ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Dar es Salaam na sare ya 1-1 Mahe, Welayta Dicha iliitoa Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, Yanga inaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa na mara ya nne kwa ujumla kihiostoria.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 ilipotolewa na na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0 iliyofungwa Khartoum baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Iliingia kwenye kapu hilo baada ya kutolewa na  Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 iliyofungwa mjini Tunis, baada ya sare 0-0 Mwanza.
Mwaka pekee Yanga ilifuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni 2016, ilipoitoa Sagrada Esperança ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola.
Hiyo ilikuwa baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 2-1 Alexandria.
Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa Kundi moja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. 
Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya MO Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam huku mechi nyingine zote nne ikifungwa, zikiwemo mbili za nyumbani na ugenini na TP Mazembe.
Mwaka jana pia Yanga baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka, ikaenda kutolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda 1-0 Dar es Sakaam na kufungwa 4-0 Algiers.
Mshindi wa jumla atajihakikishia kitita cha dola za Kimarekani, 550,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.1 za Tanzania ambazo zinaweza kuongezeka kama timu ikiingua Nusu Fainali na kuwa dola 800,000 (zaidi ya Sh. Bilioni 1.6), Dola Milioni 1.2 (zaidi ya Sh. Bilioni 2.5) kwa nafasi ya pili na Dola Milioni 2.5 (zaidi ya Sh. Bilioni 5) kwa kuchukua Kombe.
Matokeo mazuri zaidi kwa timu za Tanzania katika michuano hii ni mwaka 1993, Simba SC ilipofika fainali katika mfumo wa zamani wa mtoano mwanzo hadi mwisho na kufungwa na Stella Abidjan kwa mabao 2-0 Dar es Salaam baada ya sare ya 0-0 nchini Ivory Coast.
Kila la heri Yanga SC. Mungu ijaalie Yanga SC ishinde mechi ya leo na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Mungu ibariki Tanzania. Amin.

Monday, April 16, 2018

MSUVA AFUNGA MAWILI NA KUINUSURU JADIDA KUCHAPWA UGENINI LIGI YA MOROCCO

Image result for simon msuva 

WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva leo amefunga mabao mawili timu yake, Difaa Hassan El Jadida ikilazimisha sare ya 3-3 ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu ya Morocco dhidi ya wenyeji, Olympique de Khouribga Uwanja wa Phosphate mjini Khouribga.
Matokeo hayo yanaiongezea pointi moja Jadida na kushuka kwa nafasi moja hadi ya nne kwenye Ligi ya Morocco yenye timu 16, ikifikisha pointi zake 38 baada ya kucheza mechi 25.
Msuva amefunga mabao yake dakika za 65 na dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida, hilo likiwa bao lililoinusuru Jadidi kupoteza mechi leo na kuibuka shujaa wa timu yake, wakati bao lingine la timu hiyo limefungwa na Tarik Astati dakika ya 33.

 Mabao ya Khouribga yamefungwa na Zouhair El Moutaraji mawili dakika za nne na 38 na Adam Nafati dakika ya 55.
Kikosi cha Difaa Hassan El-Jadida kilikuwa; Aziz El Qinani, Fabrice Ngah, Youssef Aguerdoum, Tarik Astati, Mohamed Hamami, Bakary N'diaye, Marouane Hadhoudi, Bilal El Magri, Saimon Msuva, Ayoub Nanah na Mario Mandrault Bernard.

ZANZIBAR WAFUNGIWA KUSHIRIKI CECAFA U-17 KWA KUPELEKA WAKUBWA, SERENGETI YATOA SARE NA BURUNDI

Image result for karume boys 
TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Zanzibar, Karume Boys imefungiwa mwaka mmoja kushiriki michuano ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Cup U17 na kupigwa faini ya dola za Kimarekani 15,000 kwa kosa la kupeleka wachezaji waliozidi umri.
Michuano ya CECAFA Challenge Cup U17 inaendelea nchini Burundi na Zanzibar inadaiwa kuorodhesha wachezaji waliozaliwa kabla ya Januari 1 mwaka 2002, ambao wazi wamezidi umri unaotakiwa wa miaka 17.
Jana timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania Bara, Serengeti Boys ilitoa sare ya 1-1na Uganda katika mechi yake kwanza ya michuano hiyo.

Sunday, April 15, 2018

Milio ya risasi inasikika katika vijiji vya Beni DRC

Walinda amani wa Umoja wa mataifa na wanajeshi wa serikali ya Congo wanakabiliwa na mashambulio kutoka makundi kadhaa ya wanamgambo Kivu ya kaskazini
Tunapokea taarifa kwamba milio ya risasi na mizinga inasikika katika mji wa Beni kaskazini mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Duru za kuaminika zimesema waasi kutoka Uganda wa ADF wamezishambulia kambi kadhaa za jeshi la taifa hilo.
Mapigano hayo yanaripotiwa katika vijiji vya Ngadi, Boikene na Mathembo, Kaskazini mwa mji wa Beni ambapo waasi wa ADF walizishambulia kambi za jeshi kuanzia saa kumi na moja alfajiri Jumapili.

Mkuu wa jeshi anayeongoza operesheni Sokola 2 yenye lengo la kutokomeza makundi ya waasi katika eneo hilo, amethibitisha kuwa ni waasi wa ADF ndio walianzisha vita na kwamba hadi sasa ni raia mmoja amefariki, na askari mmoja amejeruhiwa.
Mkuu huyo wa jeshi Mak Azukai anasema wamemkamata mwanamgambo mmoja wa ADF.

Ameeleza kwamba ni vigumu kutoa taarifa zaidi kwa sasa kwasababu bado mapigano yanaendelea.Tangu Ijumaa, mashirika ya kiraia yalikuwa yametoa onyo kwa jeshi na vyombo vya usalama nchini humo kuhusu uwezekano wa kutokea shambulio la waasi kutokana na fununu walizokuwa nazo.

Raia wengi wamekimbilia porini na maeneo jirani kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
 Kumekuwa na mapigano kila kukicha katika miji kadha katika ukanda wa mashariki mwa DRC hasa katika mikoa ya kivu kusini na kaskazini, ambapo makundi katika maeneo hayo yaliojihami kwa silaha kama vile kundi la FDLR pamoja na ADF yameshutumiwa kwa kutatiza usalama wa raia.Mwandishi wa BBC mashariki mwa nchi hiyo anasema mji wa Beni umekuwa ukishuhudia mauwaji mara kwa mara kutokana na mashambulio ya makundi hayo ya waasi ambao hujihami kwa silaha kama bunduki, visu pamoja na mapanga na kisha kutekeleza mauajai katika vijiji vya eneo hilo.
 Allied Democratic Forces -ADF - ni kundi la wanamgambo lenye chimbuko lake nchini Uganda ambalo limekuwa likivuka mpaka kati ya mataifa mawili.

Kundi hilo linatajwa kuwa la wanamgambo wa kiislamu lakini kama ilivyo kwa makundi mengi katika eneo hilo linalokumbwa na umaskini mkubwa na ukosefu wa utulivu, sabau za kutekeleza mashambulio kama haya ni tofuati na sio tu kwa misingi ya imani
Ghasia zimeendelea kushuhudiwa Congo na kusababisha maelfu ya watu kupoteza makaazi yao huku mapigano yakishuhudiwa katika majimbo tofauti kutoka eneo linalokumbwa na ghasia kwa muda mrefu sasa mashariki hadi katika maeneo ya Kasai na Tanganyika.

Mvua kubwa Dar es Salaam yatatiza usafiri wa mabasi ya mwendokasi

Mabasi ya mwendo wa kasi TZ

Usafiri wa mabasi hayo umesitishwa kutokana na mafuriko eneo la Jangwani.
Muandishi wa BBC Mjini Dar es Salaam anaeleza kuwa kila mvua kubwa inaponyesha huduma za mabasi hayo husitishwa kutokana na sababu kadhaa.
Mojawapo ya sababu ni kufurika maji kwa njia ambazo mabasi hayo yanapitia na pia kufurika maji kwenye kituo hicho kikuu ambapo mara ya mwisho mabasi kadhaa yaliharibika sababu ya kujaa maji.
Sababu nyingine ni kukatika kwa umeme kwenye vituo vyake wakati wa mvua - hivyobasi kusababisha kukwama kwa mfumo wake wa ukataji tiketi.

Hii sio mara ya kwanza kwa mabasi hayo ya mwendo kasi yalioanza kuhudumu Tanzania mnamo Mei mwaka 2016 mjini Dar es Salaam, kukabiliwa na athari za mvua kubwa.
Mwaka jana mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha kampuni ya usafiri wa mabasi hayo - Udart, Deus Bugaywa alieleza kuathirika kwa mabasi 29 kati ya 134 baada ya maji kuingia katika sehemu tofuati za magari hayo zikiwemo injini.
Kwa sasa taarifa kutoka baadhi ya vyombo vya habari nchini zinasema huduma ya usafiri wa mabasi hayo imesitishwa kutoka na kwenda katikati ya jiji la Dar es Salaam na kwamba itarudishwa pindi hali itakapoimarika.

Sunday, April 8, 2018

Serikali Kuanzisha Kampeni Ya Jiongeze Tuwavushe Salama ili kupunguza vifo vya Mama na Mtoto

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amesema matatizo ambayo yanatokana na uzazi yapo ambayo yanaweza kuzuilika na kuhimiza wadau kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuendelea kupunguza vifo vya mama mjazito na mtoto.

Pia ametoa pongezi kwa hatua zinazochukuliwa na Taasisi ya Childbirth Survival International(CSI) ya kuhakikisha wanatoa elimu ya afya salama ya uzazi na kushiriki kwa vitendo katika kufanikisha vifo kwa mama na mtoto vinapungua hapa nchini.

Amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akitoa hotuba yake kwenye Maadhimisho ya miaka mitano ya CSI na kutumia nafasi hiyo kuwapongeza waanzilishi wa taasisi hiyo Stella Mpanda na Profesa Tausi Kagasheki.

Rais mstaafu Kikwete amesema kumekuwepo na vifo ambavyo vinatokea kwa wajawazito na watoto ambao hawana hatia na kutumia nafasi hiyo kuhimiza wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kupunguza vifo hivyo.

Amesema ipo haja ya kuendelea kutolewa elimu ambayo itasaidia jamii kutambua umuhimu wa kuhudhuria kliniki kwa mama mjazito na kubwa zaidi kuendelea kutatua changamoto zilizopo kwenye eneo la afya ya uzazi na vifo. Ameelezea hatua ambazo zinachukuliwa katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

“Nimefurahi sana kuona taasisi hii imenzishwa na akina mama wa Tanzania. Stella Mpanda yeye ni mkunga na Tausi yeye ni mwanataaluma .Nifaraja sana wamama wa Tanzania kufanya jambo kubwa kama hili la kuhakikisha wanashiriki katika kupunguza vifo vya wajawazito,

“Wametoa heshima kubwa kwa nchi yetu na pia wamefanya jambo kubwa kwa wanawake nchini kwa kuanzisha taasisi kubwa kama hii ya CSI. Kwa bahati mbaya akina mama wakati mwingine mnashindwa kupongezana. Adui wa mwanamke ni mwanamke ni mwenyewe,” amesema Rais mstaafu Kikwete.

Kuhusu changamoto zilizopo kwenye afya ya uzazi na kwamba moja ya malengo ya milenia inazungumzia kupunguza vifo vya mama mjazito na watoto chini ya miaka mitano.

“Wakati naingia madarakani mwaka 2005 , vifo kwa watoto wanaokufa ilikuwa 578 kati ya vizazi hai 100,000 wanaozaliwa. Baadae tukapunguza vifo hadi watoto 432 lakini ikapanda tena hadi vifo vya watoto 556 wakati lengo la milenia ilikuwa ni watoto 191,

“Hivyo tukaamua kuweka mikaka katika kuhakikisha tunapunguza vifo hivyo,” amesema.

Hata hivyo takwimu za mwaka 2016 kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni kwamba kati ya vizazi hai 100,000 wanaopoteza maisha ni 556.

Serikali kuja na Kampeni ya JIONGEZE TUWAVUSHE SALAMA
Kwa upande wa Waziri  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema wanatarajia kuanzisha kampeni   itakayofahamika Jiongeze tuwavushe salama.

Amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha mama mjazimto anajiongeza kwa kuhakikisha anakwenda kituo cha afya na akifika anayetoa huduma naye ajiongeze kwa kutoa huduma sahihi ambayo mtamuwezesha mjazmito kujifungua salama.

Waziri Mwalimu ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua ambazo Serikali ya awamu ya tano inavyochukua jukumu la kuhakikisha vifo vya mama mjazito na mtoto vinapungua ambako akagusia kampeni hiyo.

“Tumeongeza bajeti ya wizara ya afya na sehemu kubwa pamoja na kuangalia dawa na vifaa tiba pamoja na miundombinu pia tumeweka nguvu katika afya ya mama na mtoto,” amesema.

Wakati huo huo Mwalinzishi na Mkurugenzi wa CSI Stella Mpanda ameelezea namna ambavyo taasisi yao imejikita katika kuhakikisha vifo vya mama mjazito na mtoto vinaungua na kufafanua kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya uzazi.

Thursday, April 5, 2018

Wednesday, April 4, 2018

TWIGA STARS WABANWA NYUMBANI NA ZAMBIA, SARE 3-3 KUFUZU FAINALI ZA AFRIKA GHANA 2018


 

 

 TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) imejiweka vibaya katika kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AWC) Ghana Novemba mwaka huu kwa kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya wenzao wa Zambia (Shepolopolo) katika mechi iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Twiga Stars inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 4-4 katika mechi ya marudiano itakayofanyika mjini Lusaka, Zambia Aprili 8 mwaka huu ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo
Mabao ya Twiga Stars katika mchezo huo yalifungwa na Stumai Abdallah na Asha Rashid 'Mwalala' ambaye alipachika mawili.

Kwa upande wa Shepolopolo waliofunga ni Barbra Banda aliyefunga mawili na lingine likipachikwa na Misozu Zulu.
Hadi wanakwenda mapumziko, Twiga Stars inayofundishwa na Kocha Sebastian Mkoma na Edna Lema 'Mourinho' ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Shepolopolo ilifanya mashambulizi zaidi ukilinganisha na wenyeji lakini kipa wa Twiga Stars, Fatuma Omary, alijitahidi kudaka mashambulizi na kuisaidia timu yake katika mechi hiyo iliyochezeshwa na waamuzi kutoka Chad.
Baada ya mechi kumalizika, wachezaji wa Shepolopolo ambao walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Kenya na kufungwa 3-0, walianza kucheza "ndombolo" ishara ambao wamefurahia matokeo hayo ya ugenini ambayo kwao ni mazuri.
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zinatarajiwa kufanyika Novemba na Desemba mwaka huu jijini Accra, Ghana wakati zile za dunia zitafanyika mwakani Paris, Ufaransa.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Fatuma Omary, Wema Richard, Happy Hezron, Fatuma Issa, Sophia Mwasikili/Esther Mayala dk52, Evellyne Sekikubo, Stumai Abdallah, Deonisia Daniel, Asha Rashid ‘Mwalala’, Mwanahamisi Omar ‘Gaucho’ na Amina Ally/Christina Daudi dk75.  
Zambia; Catherine Nusinda, Margareth Belemu, Jane Chalwa/Jackline Nkole dk51, Chisamu Lwendo, Anitha Mulenga, Rhoda Chileshe, Misozi Zulu, Barbra Banda, Rachael Kundananji, Hellen Chanda na Theresia Chewa/Marry Mambwe dk46.

Hotuba ya Kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, haitasomwa bungeni

Hotuba ya Kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, haitasomwa bungeni baada ya kambi hiyo kuchelewa kuiwasilisha.

Hayo yameelezwa leo, Aprili 4 na Naibu Spika Dk Tulia Ackson dakika chache kabla ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kusoma bajeti yake.

“Kwa maelekezo yaliyotolewa na Spika Ndugai, kwa kambi ya upinzani ni kuwa upinzani wanatakiwa kuwasilisha hotuba yao siku moja kabla ya bajeti kusomwa bungeni ili kuondokana na matatizo ya kuchelewa kuzipata hotuba hizo,” amesema Dk Ackson

Waziri Majaliwa leo anawasilisha bungeni mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 mjini Dodoma.