
Tunapokea taarifa kwamba milio ya risasi na mizinga inasikika katika mji wa Beni kaskazini mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Mapigano hayo yanaripotiwa katika vijiji vya Ngadi, Boikene na Mathembo, Kaskazini mwa mji wa Beni ambapo waasi wa ADF walizishambulia kambi za jeshi kuanzia saa kumi na moja alfajiri Jumapili.
Mkuu wa jeshi anayeongoza operesheni Sokola 2 yenye lengo la kutokomeza makundi ya waasi katika eneo hilo, amethibitisha kuwa ni waasi wa ADF ndio walianzisha vita na kwamba hadi sasa ni raia mmoja amefariki, na askari mmoja amejeruhiwa.
Mkuu huyo wa jeshi Mak Azukai anasema wamemkamata mwanamgambo mmoja wa ADF.
Ameeleza kwamba ni vigumu kutoa taarifa zaidi kwa sasa kwasababu bado mapigano yanaendelea.Tangu Ijumaa, mashirika ya kiraia yalikuwa yametoa onyo kwa jeshi na vyombo vya usalama nchini humo kuhusu uwezekano wa kutokea shambulio la waasi kutokana na fununu walizokuwa nazo.
Raia wengi wamekimbilia porini na maeneo jirani kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
Kumekuwa na mapigano kila kukicha katika miji kadha katika ukanda wa mashariki mwa DRC hasa katika mikoa ya kivu kusini na kaskazini, ambapo makundi katika maeneo hayo yaliojihami kwa silaha kama vile kundi la FDLR pamoja na ADF yameshutumiwa kwa kutatiza usalama wa raia.Mwandishi wa BBC mashariki mwa nchi hiyo anasema mji wa Beni umekuwa ukishuhudia mauwaji mara kwa mara kutokana na mashambulio ya makundi hayo ya waasi ambao hujihami kwa silaha kama bunduki, visu pamoja na mapanga na kisha kutekeleza mauajai katika vijiji vya eneo hilo.
Allied Democratic Forces -ADF - ni kundi la wanamgambo lenye chimbuko lake nchini Uganda ambalo limekuwa likivuka mpaka kati ya mataifa mawili.
Kundi hilo linatajwa kuwa la wanamgambo wa kiislamu lakini kama ilivyo kwa makundi mengi katika eneo hilo linalokumbwa na umaskini mkubwa na ukosefu wa utulivu, sabau za kutekeleza mashambulio kama haya ni tofuati na sio tu kwa misingi ya imani
Ghasia zimeendelea kushuhudiwa Congo na kusababisha maelfu ya watu kupoteza makaazi yao huku mapigano yakishuhudiwa katika majimbo tofauti kutoka eneo linalokumbwa na ghasia kwa muda mrefu sasa mashariki hadi katika maeneo ya Kasai na Tanganyika.
0 Comments:
Post a Comment