TIMU
ya soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) imejiweka vibaya katika
kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika (AWC) Ghana Novemba mwaka huu kwa kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi
ya wenzao wa Zambia (Shepolopolo) katika mechi iliyofanyika jana kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Kwa
matokeo hayo, Twiga Stars inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao
4-4 katika mechi ya marudiano itakayofanyika mjini Lusaka, Zambia Aprili
8 mwaka huu ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo Mabao ya Twiga Stars katika mchezo huo yalifungwa na Stumai Abdallah na Asha Rashid 'Mwalala' ambaye alipachika mawili.
Kwa upande wa Shepolopolo waliofunga ni Barbra Banda aliyefunga mawili na lingine likipachikwa na Misozu Zulu. Hadi
wanakwenda mapumziko, Twiga Stars inayofundishwa na Kocha Sebastian
Mkoma na Edna Lema 'Mourinho' ilikuwa mbele kwa mabao 2-1. Shepolopolo
ilifanya mashambulizi zaidi ukilinganisha na wenyeji lakini kipa wa
Twiga Stars, Fatuma Omary, alijitahidi kudaka mashambulizi na kuisaidia
timu yake katika mechi hiyo iliyochezeshwa na waamuzi kutoka Chad. Baada
ya mechi kumalizika, wachezaji wa Shepolopolo ambao walicheza mechi ya
kirafiki dhidi ya Kenya na kufungwa 3-0, walianza kucheza "ndombolo"
ishara ambao wamefurahia matokeo hayo ya ugenini ambayo kwao ni mazuri. Fainali
za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zinatarajiwa kufanyika
Novemba na Desemba mwaka huu jijini Accra, Ghana wakati zile za dunia
zitafanyika mwakani Paris, Ufaransa. Kikosi
cha Tanzania kilikuwa; Fatuma Omary, Wema Richard, Happy Hezron, Fatuma
Issa, Sophia Mwasikili/Esther Mayala dk52, Evellyne Sekikubo, Stumai
Abdallah, Deonisia Daniel, Asha Rashid ‘Mwalala’, Mwanahamisi Omar
‘Gaucho’ na Amina Ally/Christina Daudi dk75. Zambia;
Catherine Nusinda, Margareth Belemu, Jane Chalwa/Jackline Nkole dk51,
Chisamu Lwendo, Anitha Mulenga, Rhoda Chileshe, Misozi Zulu, Barbra
Banda, Rachael Kundananji, Hellen Chanda na Theresia Chewa/Marry Mambwe
dk46.
0 Comments:
Post a Comment