Daktari: Serikali inahusika ARV bandia |
![]() WAKATI utata ukiendelea kugubika usambazwaji wa dawa bandia za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV), daktari katika Kitengo cha Ukimwi, Dar es Salaam ameitaka Serikali kujichunguza yenyewe, kwa kuwa dawa hizo hazisambazwi na watu binafsi. Daktari huyo, Charles Lyimo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Dawa katika Kitengo cha Ukimwi Hospitali ya Amana, alisema jana kuwa hakuna sababu ya kutafuta mchawi kwenye tatizo hilo; Serikali inahusika. “Siyo rahisi kujua kwamba hii ni dawa halisi au bandia, lakini tuna uhakika na dawa tunazotumia kwa sababu zinaagizwa na Serikali peke yake. Hakuna mtu binafsi aliyepewa tenda (zabuni) ya kuziagiza,” alisema Dk Lyimo. Dk Lyimo alisema awali, dawa hizo zilikuwa zikiagizwa kutoka Marekani, lakini baadaye utaratibu huo ukabadilishwa na zikaanza kuagizwa kutoka India. “…(Serikali) inapeleka oda kiwandani na ndiyo inayozigawa dawa hizo na kuzisambaza kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Lakini pia dawa hizi zinatengenezwa Arusha kwenye kiwanda kilichopewa kibali na Serikali,” alisema Lyimo na kuongeza: “Kama kuna dawa bandia, basi Serikali ijihoji. Kwanza mimi ninaposikia habari hizo huwa nacheka tu kwa sababu tangu sakata hili limeanza, wizara inajigongagonga tu… hawatuhusishi wala kutuuliza… na sisi tunaendelea tu kugawa dawa…” |