ATAKA IJIHOJI IJE NA MAJIBU, AELEZA ATHARI ZAKE, NAIBU WAZIRI ATAKA IPEWE MUDA ZAIDI KUCHUNGUZA TATI WAKATI
utata ukiendelea kugubika usambazwaji wa dawa bandia za kupunguza
makali ya virusi vya Ukimwi (ARV), daktari katika Kitengo cha Ukimwi,
Dar es Salaam ameitaka Serikali kujichunguza yenyewe, kwa kuwa dawa hizo
hazisambazwi na watu binafsi.
Daktari huyo, Charles Lyimo ambaye
ni Mkuu wa Idara ya Dawa katika Kitengo cha Ukimwi Hospitali ya Amana,
alisema jana kuwa hakuna sababu ya kutafuta mchawi kwenye tatizo hilo;
Serikali inahusika.
“Siyo rahisi kujua kwamba hii ni dawa halisi
au bandia, lakini tuna uhakika na dawa tunazotumia kwa sababu zinaagizwa
na Serikali peke yake. Hakuna mtu binafsi aliyepewa tenda (zabuni) ya
kuziagiza,” alisema Dk Lyimo. Dk Lyimo alisema awali, dawa hizo
zilikuwa zikiagizwa kutoka Marekani, lakini baadaye utaratibu huo
ukabadilishwa na zikaanza kuagizwa kutoka India.
“…(Serikali)
inapeleka oda kiwandani na ndiyo inayozigawa dawa hizo na kuzisambaza
kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Lakini pia dawa hizi zinatengenezwa
Arusha kwenye kiwanda kilichopewa kibali na Serikali,” alisema Lyimo na
kuongeza:
“Kama kuna dawa bandia, basi Serikali ijihoji. Kwanza
mimi ninaposikia habari hizo huwa nacheka tu kwa sababu tangu sakata
hili limeanza, wizara inajigongagonga tu… hawatuhusishi wala kutuuliza…
na sisi tunaendelea tu kugawa dawa…”
Alipotakiwa kueleza tofauti
iliyopo kati ya ARV zinazotengenezwa India na zile za Tanzania, Dk Lyimo
alisema: “Ni sawa na dawa za kutuliza maumivu za Panadol na Asprin.
Kuna wagonjwa wenye vidonda vya tumbo hawawezi kutumia Asprin, hawa
wanatumia Panadol. Vivyo hivyo kwenye Ukimwi kuna wagonjwa ambao
wanapata madhara wanapotumia dawa za India. Hawa sasa tunawapa dawa za
Tanzania.”
Dk Lyimo alisema mgonjwa anabadilishiwa ARV kulingana
na jinsi zinavyompenda au kumdhuru na ikifikia hapo, mgonjwa huyo
anahitaji uangalizi wa karibu wa daktari.
“Kuna dawa zinazonyonya
damu, nyingine zinakula nyama na nyingine zinaleta maruweruwe na njozi
mbaya. Kwa hiyo tukiona athari hizo tunambadilishia mgonjwa dawa hizo,”
alisema Dk Lyimo. Akizungumzia madai hayo, Naibu Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alikiri kuwa ni Serikali pekee
inayoagiza dawa hizo kwa ajili ya wananchi wake na akataka jamii ifahamu
pia kuwa ni Serikali hiyohiyo iliyogundua tatizo hilo na kuanza
kulifanyia kazi.
“Ni kweli Serikali pekee ndiyo inayoagiza dawa
na Serikali hiyohiyo ndiyo iliyounda TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa),
ambayo kwa kazi nzuri imefanikiwa kugundua kuwapo kwa dawa bandia. Kwa
hiyo tuwape muda wa uchunguzi,” alisema.
Hata hivyo, hakusema
itaichukua TFDA muda gani kumaliza kazi hiyo akisema: “Hii ni kazi ya
kitaalamu na inayohusisha mambo mengi. Siyo kwamba muda haujulikani,
ripoti hiyo bado iko kwenye uchunguzi na uchunguzi unachukua muda mrefu…
Tuwape muda wataalamu.”
Hata hivyo, mmiliki wa Kiwanda cha
Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPIL) kinachotengeneza dawa
hizo, Zarina Madabida alikaririwa na gazeti hili jana akisema kuwa
ndicho kilichogundua kuwapo kwa dawa hizo na kutoa taarifa kwa TFDA
kikiomba iingilie kati ili kuondoa dawa hizo bandia kwenye mzunguko.
Athari za ARV bandia Kuhusu
athari za dawa bandia, Dk Lyimo alisema mgonjwa anayezitumia hana
tofauti na mtu anayekula unga ambao kimsingi hauwezi kutibu maradhi.
“Dawa
bandia siyo lazima iwe na madhara kwa mgonjwa. Cha msingi hapo ni
kwamba mgonjwa anayetumia ARV bandia anakuwa tu hajatumia dawa kwa muda
unaotakiwa,” alisema na kuongeza:
“Mtu anaweza kutumia tu unga
kutengeneza vidonge kisha akaweka nembo kwenye makopo na kuziuza kama
ARV, hii ni kuwalaghai wagonjwa.”
“Mtu asipotumia dawa, kama CD4
zake zilikuwa zimeongezeka hadi kufikia 500, hushuka tena na wale wadudu
hupata nguvu ya kushambulia vile virutubisho vya seli. Kwanza wadudu
wale huwa wajanja zaidi na wanaweza kujibadilisha kama kinyonga. Hivyo
mgonjwa hurudiwa na magonjwa nyemelezi… ni hatari mno.”
Dk Lyimo
alisema kwa wastani hupokea kati ya wagonjwa 250 hadi 300 kwa siku
hospitalini hapo na wote huja kuchukua dawa ili kuendelea na dozi zao.
Alisema kutokana na usugu wa wadudu hao na tabia yao ya kubadilika
badilika, dawa hizo ziko katika mchanganyiko wa makundi matatu
yanayotosha kupambana nao.
“Kwa kawaida mwanadamu akiwa mzima
ana CD4 1,500. Lakini akiathiriwa na Ukimwi zinapungua kwa sababu wale
wadudu wanapoingia hushambulia virutubisho (membrane) na seli za kinga
ndani ya damu.
“Hujipenyeza kwenye seli hizo na kujibadilisha na
kufanana na seli hizo na huko ndiko wanakozaliana. Mtu anapotumia ARV,
huvilewesha virusi na kuvifanya vishindwe kuzaliana, hivyo hula na
vikishiba vinalala tu, lakini havifi,” alisema.
Alisema kutokana
na gharama kubwa ya dawa hizo, wagonjwa hushauriwa kutumia ARV wakiwa
na CD4 350, hata hivyo, wapo wanaoshindwa kuvumilia hasa kutokana na
kuandamwa na magonjwa nyemelezi hata wanapokuwa na CD4 600.
|
0 Comments:
Post a Comment