Friday, September 29, 2017

SERIKALI YAFUNGIA GAZETI LINGINE

Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la kila wiki la Raia Mwema kwa muda wa siku 90 kuanzia leo.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi amesema leo Alhamisi kuwa agizo hilo pia linahusu toleo la mtandaoni.

Dk Abbasi amesema adhabu hiyo inatokana na toleo namba 529 la Septemba 27 hadi  Oktoba 3 lililochapisha habari ya uchambuzi inayosomeka “Urais utamshinda John  Magufuli.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Raia Mwema, Jenerali Ulimwengu amesema wameambiwa sababu ya kusitishwa kwa gazeti hilo ni habari hiyo.

Ulimwengu amesema kwa sasa wanashauriana kuona ni nini cha kufanya.  

Dk Abbasi amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa, Serikali inasisitiza uchambuzi huo ni maoni ya Raia Mwema  ya haki (fair comment), hata hivyo, kwa bahati mbaya, na nia ovu, makala hiyo ilisheheni nukuu za kutunga na zisizo za kweli zikimsingizia Rais John Magufuli.

Amesema gazeti hilo pia limewahi kuonywa kwa makosa mbalimbali. 

Amesema nukuu za uongo, kutungwa na zenye nia mbaya zikidai Rais alipata kusema ni, “Suruali za zamani msizitupe, mtazihitaji baadae,” na “Watakaobaki  Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume kwelikweli.”

Dk Abbasi amesema walipotakiwa kuthibitisha wapi iwe ndani au nje ya nchi Rais alipata kutoa kauli hizo, wahariri wa Raia Mwema waliomba muda ambao walipewa. “Wakarejea na kuthibitisha kuwa hawana ushahidi huo, wakakiri kosa na kuomba radhi.”

Mkurugenzi huyo amesema bado Serikali inaamini Watanzania wakiufanyia mzaha upotoshaji wa taarifa na uchochezi katika zama hizi za Tehama amani na utulivu uliopo kwa miaka mingi utapotea na kukaribisha maafa kama ilivyotokea kwingineko duniani.

“Serikali, katika uamuzi huu, uliochukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Waziri wa Habari katika kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016, imetoa adhabu ndogo tofauti na ukubwa wa kosa kwa kuwa wahariri wa gazeti hili hawakufanya tashtiti, wamekiri kosa,” amesema.

Dk Abbasi amesema kupitia hilo, wamejifunza mambo kadhaa kuhusu changamoto za kiwango cha weledi wa uandishi wa habari nchini kiasi cha kuwalazimu kutoa ufafanuzi wa kina kwa faida ya umma na tasnia yenyewe; kwamba uandishi ni taaluma adhimu na yenye haki na wajibu vinavyopaswa kufuatwa na si kufanyiwa dhihaka.

Chanzo Mwananchi

Wednesday, September 27, 2017

ASKOFU KATOLIKI YUKO TAYARI KUITWA MCHOCHEZI

Askofu wa Kanisa Katoliki Ngara, Severin Niwemugizi amesema yuko tayari kuitwa mchochezi endapo kundi la watetezi wa haki za binadamu watachukuliwa kama wachochezi.

Askofu Niwemugiza amesema yeye kama kiongozi wa dini anaongozwa na maadili, haki na ukweli hivyo hajali namna wengine watakavyomchukulia.

Akifungua mkutano wa asasi za kiraia uliolenga kujadili kuhusu Katiba Mpya leo Jumatano, Askofu Niwemugizi amesema imefika wakati nchi inahitaji kuwa na dira nzuri.

Amesema hakuna mtetezi wa haki za binadamu anayetaka nchi iingie kwenye machafuko kwani wote lengo lao ni kuchochea maendeleo, amani na utulivu.

Askofu Niwemugizi amesema kuanza kutokea kwa matukio ya kuteka watoto, vifo katika mazingira ya kutatanisha na ongezeko la watu wasiojulikana ni ishara mbaya.
"Hizi sio dalili nzuri kwa Taifa lenye afya njema. Ni vielelezo vyenye dira mbaya. Imefika wakati tukae kama Taifa tukubaliane kuwa tunataka dira njema ambayo ni Katiba."

Amesema anatambua jitihada anazofanya Rais John Magufuli katika kupambana na ufisadi na kutaka rasilimali ziwanufaishe wanyonge lakini ni muhimu juhudi hizo zilindwe na Katiba nzuri.

"Rais anafanya mengi mazuri na alipoanza kila mmoja aliona dalili za matumaini lakini juhudi hizo zinaweza zisiwe endelevu kama hakuna ulinzi wa Katiba,”

"Tunahitaji Katiba tena Katiba nzuri ambayo haitaruhusu kuchezewa na yeyote kwa maslahi au matakwa yake binafsi."

Amesema, "Namshauri Rais achunguze kwa makini yatakayozungumzwa kwenye mkutano huu,  ayaone kuwa yana nia njema na ayafanyie kazi."

MEYA WA UBUNGO KUZUNGUMZIA SHAURI LA VYETI DHIDI YA MAKONDA

Meya wa Ubungo , Boniface Jacob ameeleza kuwa kesho atafika katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma kuzungumzia shauri lake la vyeti dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Jacob amesema wiki iliyopita amepokea barua kutoka sekretarieti wakimtaarifu kwamba wiki hii ndiyo wanalifanyia kazi shauri lake.

“Wananitaka kwamba baadhi ya mambo niliyoyaongea wananitaka na mimi nipeleke vielelezo vya ufafanuzi lakini kimsingi ni mambo mapya, yaani kana kwamba mtuhumiwa wangu mambo ya vyeti amekiri, amekubali.”

Jacob amesema akitoka kwenye mahojiano hayo na Sekretarieti ya Maadili ataongea na vyombo vya habari juu ya shauri hilo kuhusu kugushi vyeti na malalamiko mengine manne.

Mbali na hilo amesema atazungumzia vishawishi na vitisho katika kulimaliza shauri hilo lisiendelee.
“Kutoridhika na mwenendo wa shauri hilo linavyofanywa kwa kuchelewa na usiri mkubwa sana.”

Monday, September 25, 2017

TFF YAPATA UDHAMINI HUU

Shirikisho la soka nchini TFF, leo Septemba 25 limesaini mkataba na benki ya KCB wenye thamani ya shilingi 325,000,000.
 Akiongea wakati wa kusaini mkataba huo Rais wa TFF Wallace Karia amesema huo ni ushahidi kuwa shirikisho lina ushirikiano na wadau mbalimbali wa mpira nchini.

Aidha Karia amesema fedha hizo zitaelekezwa kwenye kukuza vipaji vya soka pamoja na maendeleo ya soka nchini kwa ujumla.

Huu ni mkataba mkubwa wa kwanza kusainiwa na shirikisho hilo tangu uongozi mpya chini ya Rais Wallace Karia uingie madarakani August 12 mwaka huu.

WAZIRI UMMY ASIMAMISHA MUHIMBILI KUTOA RUFAA ZA MATIBABU NJE

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa agizo kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuhakikisha haitoi rufaa ya matibabu nje ya nchi ikiwa wana uwezo wa kutibu maradhi husika hapa nchini.

Ummy amesisitiza wataalamu kutowaogopa wanasiasa ikiwa wana uwezo wa kumtibu mgonjwa hapa nchini haina ulazima wa kumwandikia rufaa nje ya nchi hata akiwa ni Rais John Magufuli.

Ametoa agizo hilo leo Jumatatu wakati akipokea msaada wa vifaa vipya kwa ajili ya vyumba viwili vya upasuaji vya watoto wadogo na wodi ya watoto ya upasuaji vyenye thamani ya Dola za Marekani 675,000 sawa na Sh1.5 bilioni,  kutoka kwa wataalamu na wahisani kutoka nchini Uingereza kupitia taasisi ya Archie Wood Foundation.

"Rais aliponiteua aliniagiza kwamba lazima niachane na rufaa za nje, hatuwezi kuachana nazo ikiwa magonjwa yanayoweza kutibiwa ndani yatatibiwa nje," amesema Ummy.

Amesema Watanzania wana imani na  Muhimbili  na hivi sasa wengi wanatoka hospitali za kulipia na kufuata matibabu ila changamoto iliyopo ni majengo lakini wapo mbioni kujenga jengo la ghorofa kwa ajili ya wagonjwa wa kulipia.

"Msitoe rufaa ya mgonjwa kama hamjajiridhisha kwamba mnaweza kumtibu hapa hata kama awe Rais, waziri au nani msitoe rufaa kwani maana yake mtakuwa mmeshindwa ni lazima ninyi mseme kwamba hamuwezi na sisi tutashughulikia," amesema.

Amewatahadharisha wataalamu hao na wanasiasa kwamba lazima wahakikishe kweli hawawezi kutibu na kwamba wizara ipo tayari na itawaunga mkono.

MANJI ATOA UTHIBITISHO WA DAWA ALIZOKUA ANATUMIA

Mfanyabiashara Yusuph Manji, leo Jumatatu amepanda kizimbani kujitetea katika shtaka linalomkabili la matumizi ya dawa za kulevya ambapo akiongozwa na Wakili wake Hajra Mungula.

Manji ameionyesha Mahakama udhibitisho uliotumwa na daktari wake kutoka Marekani kwa njia ya baruapepe wa aina ya dawa alizokuwa akitumia

MAGUFULI APIGA MARUFUKU MFANYAKAZI KUHAMISHWA BILA KULIPWA STAHIKI

Rais John Magufuli amerejea agizo lake la kupiga marufuku mfanyakazi yeyote kuhamishwa kituo cha kazi pasipo kulipwa stahiki zake.

Ametoa agizo hilo leo Jumatatu, ailpokuwa akizungumza na wananchi wa Sangsi Jijini Arusha akiwa njiani kuelekea njiani kuelekea Uwanja wa Ndege a Kimataifa wa Kilimanjaro KIA kurudi Dar es Salaam. na  kusikiliza kero zao wakiwemo wafanyakazi waliolalamika kuhamishwa vituo vya kazi bila kulipwa stahiki zao.

Rais Magufuli amemaliza ziara ya siku sita mkoani Arusha.

Akizungumzia kero za wananchi wa Pacha ya Kia waliolalamikia tatizo la uhaba wa maji, kunyang’anywa maeneo ya biashara na waliokuwa walinzi wa uwanja wa ndege kudai haki zao, Rais Magufuli ameziagiza mamlaka husika kushughulikia matatizo hayo.

Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutatua kero za wananchi na kuwahudumia bila kuwabagua kwa misingi ya itikadi za kisiasa, dini na ukabila.

Amesema katika kutimiza azma hiyo, Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Usa River - Arusha inayojengwa kwa gharama ya Sh139 bilioni; mradi wa maji wa Arusha utakaogharimu Sh42 bilioni; mradi wa kusambaza umeme katika vijiji zaidi ya 200 na mingine inayotekelezwa katika maeneo hayo.

“Nina uhakika ninyi wakazi wa Arusha mnaona inavyobadilika, kabla ya kujengwa barabara hii kulikuwa kunatokea ajali nyingi na kuna watu walikufa pale kwenye daraja, inawezekana wengine wameanza kusahau, wanaozaliwa sasa hivi wanaweza kuona haya si chochote lakini hii ni ishara ya kupanda kwa uchumi wetu, uchumi unapopanda na miundombinu inakuwa mizuri,” amesema.

MSIGWA AACHIIWA

Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mch. Peter Msigwa ameachiwa huru kwa dhamana jana usiku baada ya kukamatwa akiwa kwenye mkutano wa hadhara.
Msigwa ameachiwa baada ya kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao ni Alex Kimbe pamoja na Mwenyekiti wa Bavicha Iringa Leonce Marto , saa nne usiku 

Msigwa alishushwa jukwaani jana jioni na jeshi la polisi akiwa anahutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Mlandege Manispaa ya Iringa ambapo alikamatwa kwa kutuhumiwa kufanya uchochezi dhidi ya  vyombo vya usalama .

Inadaiwa kuwa Mchungaji Msigwa  alikuwa na kibali cha siku tatu cha kufanya mikutano katika jimbo lake na mkutano wa jana ulikuwa wa kwanza.

Marto amesema mikutano yake imefungiwa na hapaswi kuendelea na ziara yake katika kata nyingine mpaka hapo OCD atakapoamua au vinginevyo.

Leo mbunge Peter Msigwa anatakiwa kuripoti kwa RCO na huenda kesi ya uchochezi ambayo tayari imeshafunguliwa jalada lake ikapelekwa Mahakamani .

Imebainishwa kwamba mbunge huyo atazungumza na vyombo vya habari leo mchana kuweka wazi madhila yaliyompata wakati akitekeleza wajibu wake kwa wananchi.

Thursday, September 21, 2017

KIKOSI CHA SIMBA DHIDI YA MBAO LEO

Klabu ya Simba leo inashuka dimbani ikiwa ugenini jijini Mwanza dhidi ya timu ya Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mchezo ambao unachezwa katika uwanja wa CCM Kirumba.

Aishi Manula
Erasto Nyoni
Mohamed Hussen
Juuko Murushid
Method Mwanjale
James Kotei
Nicholas Gyan
Mzamiru Yassin
John Bocco
Emanuel Okwi
Shiza Kichuya

SUB
Emanuel Mseja
Ally shomari
Salim Mbonde
Jonas Mkude
Said Ndemla
Haruna Niyonzima
Juma Luizio

LORI LA DANGOTE LANASWA NA WAHAMIAJI HARAMU

Wahamiaji haramu wanane kutoka Ethiopia wamekamatwa wakisafirishwa kwa lori la kampuni ya Dangote kwenda Mtwara.

Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Edward Chegero amesema leo Alhamisi kuwa, wahamiaji hao walikamatwa Kongowe wilayani Temeke.

Amesema wamekamatwa jana Jumatano baada ya idara kupata taarifa na baadaye kuweka mtego uliowanasa.

Chegero amesema mbali na wahamiaji hao, idara imewakamata Watanzania wanne waliokuwa wakiwasindikiza wahamiaji hao.

Amesema Watanzania hao walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota Passo.

Kaimu kamishna amesema uchunguzi unaendelea ili kuwakamata wahusika wote wa mtandao huo.

Chegero amesema baadhi ya wahamiaji hao walikuwa na tiketi zinazoonyesha wanatoka Msata kwenda Dar es Salaam.

Amewataka madereva wa malori na usafiri mwingine kutosafirisha wahamiaji haramu kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja cha sheria.

Kaimu kamishna pia amewaonya wamiliki wa nyumba za wageni zinazotumika kuwaficha wahamiaji hao akisema kiama kwao kinakuja.

SERIKALI YANENA KUHUSU MATIBABU YA LISSU

Serikali imesema ipo tayari kugharamia gahrama za matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Antiphas Lissu katika hospitali yoyote duniani, iwapo familia itaomba jambo hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo na  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu , na kusema kwamba kama familia itahitaji na ripoti ya madaktari ikionyesha kuna ulazima, serikali itasimamia suala hilo.


Hivi karibuni kumekuwa kukiendeshwa kampeni ya kuchangia matibabu ya Tundu Lissu baada ya gharama zake za matibabu kuwa kubwa huku watu wakiitupia lawama serikali.